Tuesday, January 31, 2017
POMBE SIGARA CHUMVI CHANZO CHA UGONJWA WA SARATANI YA UTUMBO
POMBE SIGARA CHUMVI CHANZO CHA UGONJWA WA SARATANI YA UTUMBO
TAKWIMU
*Wagonjwa milioni 22 ifikapo h2030 ikilinganishwa na milioni 14 katika mwaka 2012. WHO
*Asilimia 80 wanafariki dunia kutokana na kuchelewa kupata huduma ya matibabu. OCRI*Watu 44,000 wanagundulika kuwa na saratani kila mwaka hapa nchini. Wizara ya Afya
Kila siku magonjwa yanazidi kuibuka duniani na kusababisha hofu . Hata hivyo maradhi mengi huchochewa na mfumo wetu wa maisha, kama aina za vyakula na starehe.
Maradhi ya saratani yameendelea kushika kasi duniani kote na kusababisha taharuki kwa watu maskini na hata matajiri. Saratani huweza kuathiri sehemu yeyote ya mwili wa binadamu.
Kwa mfano, saratani huweza kujitokeza katika utumbo wa chakula. Eneo muhimu ambalo hakuna awezaye kukwepa kulitumia na visababishi vyake vinatajwa kuwa ni mamboe tuyafanyayo kila mara katika maisha yetu.
Iko mifano mingi kama vile utumiaji wa chumvi nyingi, uvutaji wa sigara, vyakula vilivyokaushwa kwa moshi (samaki, nyama), pombe na kemikali.
Saratani ya utumbo wa chakula ni saratani ambayo hutokea katika katika kifuko cha misuli midogomidogo iliyopo kati ya eneo la juu ya tumbo na mbavu.
Eneo ambalo hupokea chakula na kusaidia kupokea na kukipeleka katika makutano ambayo husagwa na majimaji yake kuingia mwilini kwa ajili ya kusaidia mfumo mzima wa uendeshaji wa mwili.
Kwa mujibu wa watafiti wa saratani wa nchini Marekani, saratani hii haitakiwi kufananishwa na saratani nyingine ya tumbo kama vile ya ini, kongosho, utumbo mkubwa na mdogo, kwa sababu kila moja ina dalili na sababu zake.
Sababu za saratani ya utumbo
Daktari Ally Mzige, wa kliniki ya AAM, inayoshughulika na afya ya uzazi, vijana, wanawake na watoto, anazitaja sababu za saratani ya utumbo wa chakula kuwa ni pamoja na kuwa na umri mkubwa. Anasema watu wengine hupata ugonjwa huo wakiwa na umri wa miaka 55 hadi 95, lakini wengi wakiwa katika umri wa kuanzia miaka 90 na kuendelea.
Pombe na sigara
Anaitaja sababu nyingine kuwa ni matumizi ya pombe na sigara, ambayo yanatajwa kuwa ni chanzo cha saratani ya karibu aina zote. Hata hivyo, sigara huongoza kwa kusababisha saratani ya utumbo kwa kuwa unapovuta moshi na kutoa nje unameza baadhi ya kemikali bila kukusudia. Sigara inasababisha saratani ya utumbo wa chakula kwa wastani wa mtu mmoja hadi watano sawa na asilimia 20, anasema Mzige.Dawa aspirini, diclofenac, diclopar
Anaitaja sababu nyingine kuwa ni kuwa na vidonda vya tumbo vya muda mrefu na baadaye hugeuka kuwa saratani ya utumbo wa chakula. Hata hivyo matumizi ya dawa kama vile asprini, kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo ni hatari kwani kuna uwezekano mkubwa zikasababisha vidonda na kufanya damu nyingi kutoka na mgonjwa kulazimika kufanyiwa upasuaji.
Vidonda vya tumbo vya muda mrefu, kwa maana ya visivyotafutiwa tiba mapema, husababisha ugonjwa huu kwa kuwa hushambulia eneo zima la tumbo, anasema Mzige.
Chumvi
Anaitaja sababu nyingine kuwa ni mfumo wa ulaji wa chakula, huku walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu ni watu wanaotumia chakula chenye chumvi nyingi.
Kwa mfano nchini Japan saratani ya utumbo wa chakula ni ugonjwa ulioenea kutokana na mfumo wao wa chakula. Wanatumia chumvi nyingi tofauti na nchi nyingine ndiyo maana katika baadhi ya nchi ugonjwa huu ni nadra kutokea, anasema Dk Mzige.
Bakteria
Mzige anasema kuwa bakteria aina ya helicobacter pylori, ambao hadi sasa haijulikani wanatokana na nini, hushambulia na kusababisha maumivu eneo la chini ya tumbo husababisha saratani ya utumbo wa chakula mara sita zaidi ya sababu nyingine.
Anafafanua mamilioni ya watu duniani kote wameambukizwa aina hii ya bakteria, lakini hawajapata saratani ya aina hii, lakini inatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kueneza saratani ya tumbo.
Dalili za saratani ya utumbo
Kwa mujibu watafiti kutoka Taasisi ya Saratani ya Marekani (ACS), dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kupungua uzito bila kufanya mazoezi, kukosa hamu ya kula, kupata maumivu ya tumbo, kusikia maumivu ya tumbo eneo la juu ya kitovu, kujaa tumbo hata kwa kula mlo mdogo na kuvimbiwa.
Naibu mkurugenzi wa afya kutoka ACS, Leonard Lichtenfeld anazitaja dalili nyingine kuwa ni kuvimba au tumbo kujaa maji, kutapika wakati mwingine damu, kupata kichefuchefu cha mara kwa mara.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na wanafunzi kutoka katika Chuo Kikuu cha Afya cha Sweden, unaonyesha kuwa sigara ina hatari ya kuambukiza saratani ya utumbo wa chakula mara 10 zaidi ya sababu nyingine. Utafiti huo pia umeonyesha kuwa wanaotafuna tumbaku wapo kwenye hatari zaidi.
Utafiti huo pia ulibainisha kuwa pombe ina nafasi ya kuambukiza saratani ya utumbo wa chakula mara nane zaidi ya sababu nyingine.
Dk Mzige anasema kama katika familia kuna aliyewahi kupata ugonjwa wa saratani ya utumbo wa chakula ipo hatari kwa wanafamilia wengine kupata ugonjwa huo, Anazitaja sababu nyingine kuwa ni kundi la damu ambapo watu walio na kundi A wapo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo ingawa ni kwa asilimia ndogo sana.
Anaendelea kueleza kuwa siyo jambo la ajabu kwa mgonjwa wa saratani wa aina nyingine kupata saratani aina hii.
Wanaofanya kazi katika maeneo ambayo wanatumia dawa kali kwa wingi, hufanya hivyo bila kupata ushauri wa daktari. Hawa hubadilisha au kuongeza homoni mwilini pamoja na matumizi ya pilipili kuwa ni miongoni sababu zinazoweza kumfanya mtumiaji kupata ugonjwa huu.
Sababu zipo nyingi, lakini kuna zile ambazo ni rahisi kuziepuka. Mara nyingi saratani aina hii inahitaji umakini mkubwa katika matumizi ya vyakula ikiwamo dawa za mitishamba ambazo ukitumia kwa muda mrefu husababisha vidonda vya tumbo na hatimye saratani ya utumbo wa chakula, anasema Dk Mzige.
Suluhisho
Dk Jaffer Dharsee, ambaye ni mkurugenzi wa tiba na mionzi wa Hospitali ya Aga Khan, anasema kuwa ni rahisi kujikinga na saratani ya tumbo kama kila mtu atakuwa makini, hasa katika vyakula.
Hakuna dawa ya kujikinga na ugonjwa huu zaidi ya kula kwa mpangilio maalum, kufanya mazoezi, kuacha matumizi ya kunywa vitu vikali kama vile pombe, uvutaji wa sigara na kula vyakula vilivyoivishwa na mafuta kwa maana ya kukaangwa,anasema Dk Dharsee.
Dk Mzige anaeleza jinsi ya kujikinga na vidonda vya tumbo ambavyo vinatajwa kusababisha ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kuepuka msongo wa mawazo ambao husababisha vidonda.
Utumbo wa chakula hauhitaji misukosuko, kunywa pombe, msongo wa mawazo, uvutaji sigara, kuchelewa kula, yaani kukaa muda mrefu bila kula. Hizo ni sababu zinazoweza kusababisha ugonjwa wa tumbo ambao una uhusiano wa karibu na ugonjwa huu. Hivyo ni bora kuepukana na vitu hivyo, anasema Dk Mzige.
Hospitali ya Aga Khan inajipanga kukabiliana na tatizo la saratani.
Mtendaji mkuu wa hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh anasema kutokana na ongezeko la wagonjwa wa saratani, wanajipanga kusogeza huduma ya matibabu na vipimo karibu na wananchi.
Anasema wametenga kiasi cha Sh12.4 bilioni, ambazo ni kwa ajili ya kupeleke huduma kwa wagonjwa popote walipo Tanzania, badala ya kutoka huko waliko na kuzifuata jijini Dar es Salaam.
Saratani ni tishio duniani kote kwa sasa, lakini katika nchi za Afrika limekuwa tishio zaidi kutokana na kukosa tiba kwa wakati au kuzipata mbali na matokeo yake mgonjwa anagundulika akiwa katika hatua za mwisho au akiwa hawezekani kutibika, anasema na kuongeza:
Lakini kwa mpango huu wa kuhakikisha tunajenga vituo vya afya katika kila mkoa vikiwa na huduma muhimu hasa tiba za ugonjwa huu, na kuwa na madaktari waliobobea, tutapunguza au kuyabaini katika hatua za awali na hatimaye wagonjwa kupata tiba mapema.
Available link for download